Maximo amuita Chove Timu ya Taifa

February 20, 2010

KOCHA Mkuu wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, Marcio Maximo, ametangaza kikosi cha wachezaji 23 kwa ajili ya mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Uganda ‘The Cranes’, itakayopigwa Machi 3, mwaka huu jijini Mwanza huku kipa wa JKT Ruvu, Jackson Chove akimjumuisha kwa mara ya kwanza.

Mbali na kutangaza kikosi hicho, ametangaza rasmi kustaafu kwa beki wa timu ya Azam FC na timu hiyo, Salum Sued ambaye ameomba kupumzika na kutoa nafasi kwa vijana chipukizi kuonesha uwezo wao.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Maximo, alisema kikosi hicho kitaingia kambini Ijumaa usiku na Jumamosi watakwenda jijini Mwanza kwa ajili ya maandalizi ya mchezo huo.

Aliwataja wachezaji hao na timu wanazotoka katika mabano ni makipa, Shabaan Shaaban ‘Kado’ (Mtibwa Sugar) na Jackson Chove (JKT Ruvu), mabeki ni Shadrack Nsajigwa na Nadir Haroub (Yanga), Salum Kanoni, Juma Jabu, Kelvin Yondani na David Naftari (Simba), Stephano Mwasika (Moro United) na Aggrey Morris (Azam FC).

Wengine ni Abdulhalim Humuod na Shaaban Nditi (Mtibwa), Erasto Nyoni (Azam), Juma Nyoso (Simba), Abdi Kassim, Kigi Makasi na Nurdin Bakari (Yanga), Mbwana Samatta (African Lyon) na Ibrahim Mwaipopo (Azam) na washmabuliaji ni Mussa Hassan ‘Mgosi’ (Simba), Mrisho Ngassa na Jerson Tegete (Yanga) John Bocco (Azam).

Wakati huohuo, Maximo aliongeza kwamba, nahodha wa timu hiyo, Salum Sued, ameomba kustaafu kuitumikia timu ya taifa ili atoe nafasi kwa wachezaji chipukizi kuonesha uwezo wao.

Alisema kutokana na Sued kuamua mwenyewe kufanya hivyo, hana pingamizi na hilo kwani katika kipindi chote alichofundisha cha miaka miwili na nusu, kwake alikuwa mtu muhimu katika safu ya ulinzi na mchango wake umeonekana.

Katika hatua nyingine, Kampuni ya Mohamed Enterprises, imetoa maji katoni 50 na mipira 15 kwa ajili ya timu ya Taifa ya wanawake (Twiga Stars) iliyo kambini kujiandaa na michuano ya kuwania fainali za Afrika zitakazofanyika baadaye mwaka huu nchini Afrika Kusini.

Na Frank Balile


Stars yainyoa New zealand 2-1

June 4, 2009

b13

Kikosi cha Taifa Stars kilicho wanyoa Netherland jana

Timu ya Taifa Taifa Stars usiku wa kuamkia leo imewapa zawadi watanzania baada ya kuichapa timu ya Taifa ya New zealand kwa mabao 2-1. Katika mchezo huo uliochezwa Uwanja Mpya wa Taifa, Taifa Stars ilikuwa ya kwanza kufungwa bao ambalo lilipatikana dakika ya 10 baada ya beki wa Stars kuunawa mpira ndani ya box, Muda mchache baadaye Stars walisawazisha kwa bao safi la kichwa lililopachikwa na mchezaji Jerry Tegete.

Mchezo huo ambao ulihudhuriwa na mamia ya mashabiki na kurushwa Live duniani kote ulikuwa wa pande zote kwani timu zilishambuliana kwa zamu na kama si makosa ya hapa na pale basi wallah tungewaumia. Bao la pili la Stars lilifungwa na mshambuliaji anayekuja juu Mwinyi Kazimoto. Mpaka kipyenga cha mwisho Taifa Stars 2-1 New zealand.

Shukrani kwa mdau wangu Robert Mwafrika kwa habari hii, Picha na Michuzi.


New Zealand yataka mechi na Taifa Stars irushwe moja kwa moja!!

May 20, 2009

 

Dar

Jiji la Dar Es Salaam ambako mechi hiyo itachezewa, Utalii si wanyama tuu tuna mengi ya kuyatangaza.

WAGENI wa Taifa Stars, New Zealand wametaka mechi baina ya timu hizo irushwe hewani laivu kati ya saa 12 jioni au 1.00 usiku kwa lengo la kuitangaza Tanzania nje ukiwamo pia Uwanja wa Taifa nchini kwao.

Wakati hilo lilifanyika, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limetangaza viingilio katika mchezo huo kuwa ni Sh40,000 kwa kiwango cha juu na cha chini kikiwa Sh 3,000.

Viingilio vingine, kulingana na TFF ni Sh 5,000 kwa mzunguko rangi ya bluu, Sh10,000 kwa jukwaa la rangi ya machungwa nyuma ya magoli na Sh15,000, rangi ya machungwa mkabala na jukwaa kuu wakati VIP C Sh20,000 na VIP B itakuwa Sh 30,000.

Gonga hapa kwa habari zaidi


Taifa Stars yaichapa Ivory Coast 1-0

February 26, 2009

Goli la Mrisho Ngasa limewapa matumaini watanzania kwa timu yao kusonga mbele ingawa bado ina mechi moja mkononi.

TAifa stars huku ikicheza kwa kujiamini imewatoa nishai wenyeji wa michuano hiyo Ivory coast kwa kuwachama bao moja bila majibu kwenye mchezo uliochezwa hapo jana.

Wachezaji mahiri wa Ivory Coast kama Karamoko Alassane, Guehi Kouko na N’gossan Antoine waliisumbua sana ngome ya Stars na walishangiliwa kwa nguvu kila waliposhika mpira.

Kwa mujibu wa matangazo ya Television iliyokuwa inaonyesha live kwenye mtandao Taifa Stars walionyesha kuumudu na mara kwa mara mtangazaji alikuwa akisema Taifa Stars walionyesha kiwango cha hali ya juu tofauti na alivyoifahamu.

KWa sasa TAifa Stars inahitaji kushinda na msemo wa adui muombee njaa ndio pahala pale kwani Taifa Starz ikishinda itakuwa na Point 6 au ikitoa Droo itakuwa na point 4 na hivyo kuipiku Zambia na Senegal.

kikosi cha mauaji

Mechi ya ufunguzi TAifa Stars ilipoteza mchezo kwa Senegal ikafungwa kwa taabu 1-0.

Kocha Maximo amesema kuwa anaauhakika vijana wake watafika mbali kwani wamezoea mashindano kwa sasa.

Go stars gooooo!!!


Tifa Stars yapoteza mchezo wa kwanza 1-0

February 22, 2009

Mpira umekwisha kati ya Taifa Stars na Senegal huko Abdijan na matokeo ni kwamba tumepewa kimoja bila majibu.

No sweat bado nafasi tunayo kwani tutacheza na wenyeji ambao washakula mabao matatu toka kwa Zambia kwenye mechi ya ufunguzi.


JK mwanamichezo basi tuu tunamuangusha.

February 11, 2009
Rais JK katika picha ya pamoja na Taifa stars baada ya dina la mchana Ikulu jana.
Rais alitumia muda huo kuwakumbusha wachezaji hao umuhimu wa michuano hiyo kwa Taifa na umuhimu wa wao kushinda, aidha JK aliwataka wachezaji hao kutozihofia timu zenye majina makubwa kwani wafanye kama kimya kingi chenye kishindo kikuu.
Picha kwa hisani ya Issa Michuzi.

Maximo alia Yanga wamemnyima wachezaji kujiunga na Taifa Stars

February 9, 2009

Kocha wa Timu ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars Marcio Maximo amesema kuwa analia na timu ya Yanga ambayo imekatalia wachezaji wake 10 kujiunga na timu ya Taifa kwa ajili ya mchezo wa majaribio na Zimbabwe.

Akionge na BBC Maximo amesema kuwa Yanga ambao wamempa sababu ya kujiandaa kwao na mechi ya Marudiano na Mauritius ambayo wiki iliyopita waliwachapa bao 8-1.

Maximo amesema kuwa YAnga imesema haiwezi kumpa wachezaji hao wote ambao yeye binafsi anasema anawahitaji sana.

Aidha kocha MAximo alisema timu yake haiigopi michuano ya kimataifa ambayo Taifa Stars itashiriki ikiwa ni michuano ya Afrioca kwa wachezaji wanaocheza ligi ya nyumbani.

Tanzania ambayo imepangwa kundi la kifo linalozishirikisha Zambia na Senegal na Ivory Coast inahitaji mazezi na mechi nyingi za majaribio kwa ajili ya kuzikabili timu hizo, akiongelea juu ya hilo Maximo amesema kuwa uzoefu ndio kilio chake kwa Timu ya Taifa kwani haina mechi nyingi za kimataifa na wachezaji wengi si wazoefu wa ichezo ya kimataifa.

Hali kadhalika MAximo amesema kuwa anafuraha kwa sasa ngalao timu kubwa zimeanza hata kutupia macho Tanzania na anasema hii ni nafasi pekee kwa wachezaji hao kujiuza kimataifa kwa kupitia michuano hii.


Tanzania 4 – 1 Mauritius

September 6, 2008

Kikosi cha Taifa Stars

Kikosi cha Taifa Stars

Tanzania kipofu kaona mwezi leo!!, Timu ya Taifa Stars imeinyuka bila huruma timu ya Taifa ya Mauritius kwa mabao 4-1 katika mchezo wao wa awali wa makundi uliofanyika huko Mauritius jumamosi 6 Sept 2008.

Mabao yote matano yalipatikana katika kipindi cha kwanza cha mchezo ndani ya dakika 22 lakini walikuwa  ni Taifa Stars waliocheza mchezo mzuri na pasi za kuonana kufanya kushangiliwa kila waliposhika mpira na mashabiki waliokuwepo uwanjani.

Alikuwa ni Shadrack Nsajigwa aliyepachika bao la kwanza lakini bao hilo lilidumu kwa sekunde 56 tuu kwani Mauritious walisawazisha kupitia kwa mchezaji wao mwenye makeke Wesley Marquette.

baadaye Tanzania walicheza kwa kushambulia zaidi na alikuwa ni Nizzar Khalfan baada ya kuandamwa lango la Mauritious aliinua furaha ya watanzania kwa kupachika bao la pili la  kuongoza kabla ya mchezaji aliyewika  Jerson Tegete kupachika mabao mawili ya mwisho. Ushindi huu wa leo umeiweesha Taifa Stars kufikisha Point 5 ikiwa bado na mechi moja mkononi. hii ina maana kuwa tunaweza kuipita Cape Verde ambayo inashika nafasi ya pili kwenye kundi letu ikiwa na Point tisa (9). Mauritius watamaliza wakiwa wa mwisho kwani wana Point moja mpaka sasa na mchezo wa mwisho wanacheza na Cameroo ambao wanaongoza kundi hili.


Stars kuivaa Mauritius kwao!

August 28, 2008
Wachezaji wa Taifa Stars walipocheza na Ghana majuzi

Wachezaji wa Taifa Stars walipocheza na Ghana majuzi

TIMU ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ inatarajia kuondoka nchini Septemba 5 kuelekea Mauritius kwa ajili ya mchezo wa marudiano dhidi ya timu hiyo kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Fredrick Mwakalebela, timu hiyo itaingia kambini kesho na itaondoka na kikosi cha wachezaji 22.

Naye Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mbrazili, Marcio Maximo alisema kikosi kitakachoingia kambini ni kile kilichochoteuliwa wakati wa mchezo wa kirafiki dhidi ya Ghana wiki moja iliyopita.

Alisema baada ya mchezo huo atakipangua kikosi ambacho kitavaana na Cape Verde, kabla ya kutaja kitakachocheza na Sudanu katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza soka la ndani.

Alisema mchezo dhidi ya Mauritius ni mgumu kwa kuwa timu hiyo itacheza nyumbani huku ikiwa na wachezaji wengi wanaocheza soka la kulipwa na kwamba ingawa Taifa Stars haina nafasi ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia bado itacheza kwa nguvu kusaka ushindi.

Source: Majira


Maximo awatema Babi, Gabriel, Ulimboka

August 12, 2008

KOCHA Mkuu wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, Marcio Maximo jana alitangaza kikosi cha wachezaji 20 kwa ajili ya mchezo wa kirafiki wa Agosti 20 mwaka huu, dhidi ya Ghana ‘Black Stars’, huku akiwatema Abdi Kassim ‘Babi’, Ulimboka Mwakingwe na Emmanuel Gabriel.

Katika kikosi hicho amemuita mshambuliaji wa Simba, aliyeng’ara katika mashindano ya Kombe la Kagame Mussa Hassan ‘Mgosi’ na kipa wa Simba, Amani Simba, ambaye hiyo ni mara ya kwanza tangu kocha huyo aje nchini mwaka 2006 kumuita kwenye kikosi chake, wakati Mgosi alienguliwa baada ya Stars kurejea kutoka Senegali katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Afrika Machi mwaka jana na kubugizwa mabao 4-0.

Sura mpya nyingine katika kikosi hicho ni kiungo wa Simba Jabir Aziz aliyeitwa kwa mara ya kwanza, wakati mshambuliaji wa Simba, Adam Kingwande naye ameitwa tena katika kikosi hicho, ambapo awali alimuita mapema mwaka huu, wakati akichezea Ashanti United, lakini akamtema siku chache baadaye.

Ukiacha Ulimboka, Babi na Gabriel mchezaji mwingine aliyeachwa ambaye alikuwa katika kikosi cha Stars kilichocheza michuano ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia dhidi ya Kameruni, Mauritius na Cape Verde ni beki Stephen Mwasika wa Prisons na kipa Shaaban Dihile (JKT Ruvu). Read the rest of this entry »


Maximo kuelekeza nguvu Kombe la Mataifa ya Afrika

July 21, 2008

KOCHA wa Taifa Stars, Marcio Maximo amesema hatawatumia wachezaji Danny Mrwanda na Erasto Nyoni kwenye mechi zilizobaki za kufuzu kucheza fainali za kombe la Dunia 2010.

Stars yenye pointi mbili kwenye kundi la kwanza linaloongozwa na Cameroon yenyev pointi 10, imesaliwa na mechi mbili dhidi ya Cape Verde na Mauritius na haina nafasi ya kusonga mbele.

Maximo alisema jijini Dar es Salaam juzi kwamba kwa hali ilivyo sasa atatumia michezo hiyo kwa ajili ya kuisuka zaidi timu yake kwa michezo miwili ya mwisho dhidi ya Sudan ya kufuzu fainali za kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani.

“Sitawatumia hao wachezaji wa nje ili kutoa nafasi kwa hawa wachezaji wa ndani ambao ndio wana kazi kubwa sasa kwenye mechi dhidi ya Sudan, nataka mpaka Novemba niwe na kikosi imara zaidi,”alisema Maximo ambaye alikuwa mapumziko Brazil.

“Nimewahi kuja ili niangalie haya mashindano ya Kagame yanayoendelea ninaamini timu zilizokuja ni ngumu na naweza kupata nafasi ya kuwaona zaidi wachezaji wa hizi klabu za Simba, Yanga na Miembeni,”alisisitiza Maximo ambaye klabu ya Yanga imepanga kumuuza kwa St.Georges ya Ethiopia kipa wake namba moja, Ivo Mapunda.

“Nataka kuangalia ni nani naweza kumuongeza kwa ajili ya kuisadia timu kwenye mechi zetu na Sudan Novemba, ndio kazi kubwa iliyobaki mbele yetu, pamoja tutafika,”alisema Maximo ambaye timu yake iliingia kwenye nafasi hiyo baada ya kuzitoa Uganda na Kenya.

Mrwanda anacheza kwenye klabu ya Al-tadhamon ya Kuwait huku Nyoni akiichezea Vital’o ya Burundi ambayo jana jioni ilikwaana na Simba kwenye michuano ya Kagame inayoendelea jijini Dar es Salaam.

Endapo Stars itaipata sare au kuifunga Sudan ugenini itakakoanzia na kushinda mchezo wa marudiano kwenye uwanja wa Taifa itafuzu kucheza fainali za michuano hiyo mipya, Januari mwaka nchini Ivory Coast.


JK Iko wapi Real Madrid?

July 18, 2008
Rais Kikwete akiwa katika moja ya mechi za Taifa stars.

Rais Kikwete akiwa katika moja ya mechi za Taifa stars.

Tumezoea kupewa ahadi mara nyingi kitu kikitokea ambapo utekelezaji wake unakuwa ama wa kusua sua au kutotekelezwa kabisa. katika Makala hii ya J Saria wa Tanzania Sports, aliiandika mwezi Juni, pamoja na mambo mengine ni kujadili jinsi gani tunaweza kufanya mbadala wa hawa Real MAdrid na kuwapa raha watanzania.

RAIS Jakaya Kikwete, aliwagusa wengi mwaka jana baada ya kuripotiwa juu ya ujio wa klabu kongwe, tajiri na yenye kila aina ya utukufu katika medani ya soka duniani, Real Madrid ya Hispania.

Ilielezwa ingekuja Julai mwaka jana ikiwa na nyota wake kama Ronaldo de Lima (sasa yuko AC Milan ya Italia), Robinho, Raul Gonzalez, David Beckham (amehamia LA Galaxy ya Los Angeles, Marekani), Roberto Carlos (amekimbilia Uturuki), na wengine wengi.

Baada ya wengine kupanguka, hakika Real Madrid inayonolewa na Bernd Schuster bado hazina ya mastaa kama kipa na nahodha wa Hispania, Iker Casillas, mabeki Fabio Cannavaro, Michel Salgado, Sergio Ramos, Pepe, Gabriel Heinze, viungo Mahamadou Diarra, Raul, Fernando Gago, Arjen Robben, Guti, washambuliaji Ruud van Nistelrooy, Javier Saviola na wengine.

Kwa hakika, hamasa ilikuwa kubwa ajabu, na mambo yalizidi kuvutia baada ya kuundwa timu maalumu ya uratibu kwa ajili ya kuwezesha ujio wa msafara wa mastaa halisi wa soka duniani, wapambe na viongozi, wote wakifikia 80!

Mbali ya kuwasafirisha, gharama za kuishi, kutalii nchini, na posho ya mechi, ilikuwa juu ya wenyeji! Mzigo mkubwa.

Hapo ndipo wachambuzi wa mambo wakaanza kuhoji kiburi cha kuubeba msalaba huo, kwa ziara ambayo nchi isingenufaika sana, zaidi ya kukamuliwa vijisenti vyetu.

Ama kwa ugumu wa kukusanya fedha, au kwa sababu nyingine, tukaarifiwa ziara haitawezekana kwa mwaka 2007 kutokana na wenyeji kuchelewa kupata mwaliko!

Mwaliko? Ndiyo, ingawa ni hao hao Real Madrid tulioambiwa kwamba wamekubali kutua nchini.

Na baadaye ikaelezwa kwamba, sasa piga ua ziara yao haitakuwa ya shaka mwakani (mwaka huu wa 2008), mara tu baada ya kumalizika kwa msimu wa Ligi Kuu ya Hispania `La Liga’ na michuano ya ubingwa wa Ulaya.

Ikawa siku, ikawa sasa, wiki, miezi na sasa mwaka, lakini hakuna aliyesikia tena habari za ujio wa Real Madrid.

Nathubutu kusema kwamba, Watanzania hawasikitiki hata chembe kutokana na ukimya wa serikali juu ya ziara ya Real Madrid.

Pengine tunapaswa kumkumbusha Rais Kikwete kwamba, dhamira yake tunaikubali, tena sana.

Hata hivyo, badala ya kugeukia klabu, licha ya umaarufu wake, tunamuomba ageukia upande wa pili, kwa kutumia kamati ya uratibu kukusanya fedha kwa ajili ya michuano maalumu itakayojumuisha Taifa Stars.

Mathalani, hata kama Real Madrid wakitua, tuna uhakika hawatacheza zaidi ya mechi moja. Kwa mtaji huu, Taifa Stars itanufaika na nini zaidi ya kupiga picha na wachezaji?

Lakini kwa fedha hizo hizo, au pengine pungufu ya hapo, yaweza kuandaliwa michuano itakayoshirikisha nchi tano za Afrika zilizocheza fainali zilizopita za Kombe la Dunia.

Kama Tanzania itakuwa na ujasiri huo na kuzipata Ivory Coast yenye nyota kama Didier Drogba, Kolo Toure, Yaya Toure, Aruna Dindane, Salomon Kalou na wengine, au Ghana yenye Michael Essien na wenzake, Angola, Togo ikiwa na Emmanuel Adebayor na Tunisia, hakuna shaka itakuwa habari kubwa.

Kwa kunogesha michuano, Cameroon na Nigeria zinaweza kualikwa, hivyo kuipa uhai zaidi michuano hiyo.

Hakika faida za michuano hiyo maalum zitakuwa kubwa mno kwa Taifa Stars ambayo ndiyo kwanza inakomaa na inahitaji kujiamini zaidi kwa kucheza mechi ngumu, kubwa na zenye mkusanyiko halisi wa nyota wa soka.

Aidha, gharama ya kuzialika nchi hizo zinaweza kurudi kupitia viingilio kutokana na kila nchi kuwa na mvuto wa aina yake, mashabiki wakitaka kupigana vikumbo kujionea nyota wanaowasikia, kuwasoma au kuwaona kupitia luninga katika ligi kubwa za Ulaya na kwingineko.

Na zaidi ya yote, kwa kuwakusanya nyota wa nchi mbalimbali labda kwa michuano ya wiki moja au mbili, nchi itakuwa imejitangaza mno kitalii.

Haya yakiwezekana, hakutakuwa na shaka kwamba, ujasiri wa Stars katika kukabiliana na mechi ngumu utaongezeka, hivyo kuiweka nchi katika nafasi nzuri ya kurudisha heshima, tukianzia na mwaka 2012 katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika na baadaye mwaka 2014 katika Kombe la Dunia.

Kinyume cha hapo, tutaendelea kuziota fainali za michuano mikubwa duniani na kubakiwa na historia ya mwaka 1980 tu.

Ndiyo maana tunasema, baada ya Real Madrid kuota mbawa, kuna njia mbadala ya kuiimarisa Stars hata kama kwa sasa haina jeuri tena ya kucheza fainali za mwaka 2010 za Mataifa ya Afrika na hata Kombe la Dunia.


%d bloggers like this: