Maximo amuita Chove Timu ya Taifa

February 20, 2010

KOCHA Mkuu wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, Marcio Maximo, ametangaza kikosi cha wachezaji 23 kwa ajili ya mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Uganda ‘The Cranes’, itakayopigwa Machi 3, mwaka huu jijini Mwanza huku kipa wa JKT Ruvu, Jackson Chove akimjumuisha kwa mara ya kwanza.

Mbali na kutangaza kikosi hicho, ametangaza rasmi kustaafu kwa beki wa timu ya Azam FC na timu hiyo, Salum Sued ambaye ameomba kupumzika na kutoa nafasi kwa vijana chipukizi kuonesha uwezo wao.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Maximo, alisema kikosi hicho kitaingia kambini Ijumaa usiku na Jumamosi watakwenda jijini Mwanza kwa ajili ya maandalizi ya mchezo huo.

Aliwataja wachezaji hao na timu wanazotoka katika mabano ni makipa, Shabaan Shaaban ‘Kado’ (Mtibwa Sugar) na Jackson Chove (JKT Ruvu), mabeki ni Shadrack Nsajigwa na Nadir Haroub (Yanga), Salum Kanoni, Juma Jabu, Kelvin Yondani na David Naftari (Simba), Stephano Mwasika (Moro United) na Aggrey Morris (Azam FC).

Wengine ni Abdulhalim Humuod na Shaaban Nditi (Mtibwa), Erasto Nyoni (Azam), Juma Nyoso (Simba), Abdi Kassim, Kigi Makasi na Nurdin Bakari (Yanga), Mbwana Samatta (African Lyon) na Ibrahim Mwaipopo (Azam) na washmabuliaji ni Mussa Hassan ‘Mgosi’ (Simba), Mrisho Ngassa na Jerson Tegete (Yanga) John Bocco (Azam).

Wakati huohuo, Maximo aliongeza kwamba, nahodha wa timu hiyo, Salum Sued, ameomba kustaafu kuitumikia timu ya taifa ili atoe nafasi kwa wachezaji chipukizi kuonesha uwezo wao.

Alisema kutokana na Sued kuamua mwenyewe kufanya hivyo, hana pingamizi na hilo kwani katika kipindi chote alichofundisha cha miaka miwili na nusu, kwake alikuwa mtu muhimu katika safu ya ulinzi na mchango wake umeonekana.

Katika hatua nyingine, Kampuni ya Mohamed Enterprises, imetoa maji katoni 50 na mipira 15 kwa ajili ya timu ya Taifa ya wanawake (Twiga Stars) iliyo kambini kujiandaa na michuano ya kuwania fainali za Afrika zitakazofanyika baadaye mwaka huu nchini Afrika Kusini.

Na Frank Balile


JK mwanamichezo basi tuu tunamuangusha.

February 11, 2009
Rais JK katika picha ya pamoja na Taifa stars baada ya dina la mchana Ikulu jana.
Rais alitumia muda huo kuwakumbusha wachezaji hao umuhimu wa michuano hiyo kwa Taifa na umuhimu wa wao kushinda, aidha JK aliwataka wachezaji hao kutozihofia timu zenye majina makubwa kwani wafanye kama kimya kingi chenye kishindo kikuu.
Picha kwa hisani ya Issa Michuzi.

Maximo kuelekeza nguvu Kombe la Mataifa ya Afrika

July 21, 2008

KOCHA wa Taifa Stars, Marcio Maximo amesema hatawatumia wachezaji Danny Mrwanda na Erasto Nyoni kwenye mechi zilizobaki za kufuzu kucheza fainali za kombe la Dunia 2010.

Stars yenye pointi mbili kwenye kundi la kwanza linaloongozwa na Cameroon yenyev pointi 10, imesaliwa na mechi mbili dhidi ya Cape Verde na Mauritius na haina nafasi ya kusonga mbele.

Maximo alisema jijini Dar es Salaam juzi kwamba kwa hali ilivyo sasa atatumia michezo hiyo kwa ajili ya kuisuka zaidi timu yake kwa michezo miwili ya mwisho dhidi ya Sudan ya kufuzu fainali za kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani.

“Sitawatumia hao wachezaji wa nje ili kutoa nafasi kwa hawa wachezaji wa ndani ambao ndio wana kazi kubwa sasa kwenye mechi dhidi ya Sudan, nataka mpaka Novemba niwe na kikosi imara zaidi,”alisema Maximo ambaye alikuwa mapumziko Brazil.

“Nimewahi kuja ili niangalie haya mashindano ya Kagame yanayoendelea ninaamini timu zilizokuja ni ngumu na naweza kupata nafasi ya kuwaona zaidi wachezaji wa hizi klabu za Simba, Yanga na Miembeni,”alisisitiza Maximo ambaye klabu ya Yanga imepanga kumuuza kwa St.Georges ya Ethiopia kipa wake namba moja, Ivo Mapunda.

“Nataka kuangalia ni nani naweza kumuongeza kwa ajili ya kuisadia timu kwenye mechi zetu na Sudan Novemba, ndio kazi kubwa iliyobaki mbele yetu, pamoja tutafika,”alisema Maximo ambaye timu yake iliingia kwenye nafasi hiyo baada ya kuzitoa Uganda na Kenya.

Mrwanda anacheza kwenye klabu ya Al-tadhamon ya Kuwait huku Nyoni akiichezea Vital’o ya Burundi ambayo jana jioni ilikwaana na Simba kwenye michuano ya Kagame inayoendelea jijini Dar es Salaam.

Endapo Stars itaipata sare au kuifunga Sudan ugenini itakakoanzia na kushinda mchezo wa marudiano kwenye uwanja wa Taifa itafuzu kucheza fainali za michuano hiyo mipya, Januari mwaka nchini Ivory Coast.


%d bloggers like this: