Ya Jay Dee, Ruge na Kusaga yanazungumzika.

May 2, 2013

jaydeecloud

Kwa takribani siku mbili mitandao ya kijamii na vyombo vya habari vimekuwa na mijadala juu ya tamko la Lady Jay Dee kama Usia wake ikitokea ametangulia mbele za haki kabla ya aliowaita wabaya wake Ruge na Kusaga.

Katika Usia huo (gonga hapa kuusoma) Lady Jay Dee ametanabaisha kinaga ubaga pasi kuficha maneno kuwa ikitokea amefariki basi Clouds FM isitangaze kifo chake, Kupiga nyimbo zake, wala ma boss wake akiwemo Ruge na Kusaga wasifike msibani na kama wakija basi wapigwe mawe.

Sio vizuri kama mpenda burudani hasa muziki wetu wa Bongo nikikaa kimya na najiona ninalo la kusema inapotokea hali kama hii, kwa mujibu wa Jay Dee uadui kati yake na Ruge ulianza pale alipojitoa kwenye Label ya Smooth Vibes ambayo ilikuwa inasimamia kazi zake ambayo ilikuwa chini ya Ruge na yeye pia kujitoa kwenye ziara za Tamasha la Fiesta kwa alichosema kulipwa ujira mdogo.

Tofauti hizi ni hatari hasa kwa sekta ya burudani na wasanii kiujumla kwani kunakuwa na mgawanyiko na kuwatia uwoga wasanii wale ambao wanahisi wangetaka kumshirikisha Sugu kwa namna yeyote iwe kikazi au kimawazo kwani kufanya hivyo ni hatari kwa kazi zao kisanii ama kwa kuogopa kuingia kwenye malumbano au kwa nyimbo zao kutopigwa redioni au kwenye TV Stesheni kabisa. Ni wazi kuwa hakuna kituo cha redio kinachomilikiwa na Clouds Media Group kinaweza kucheza wimbo wowote wa Lady Jay Dee kwa sasa, hapo ndipo tulipofikia na huo ni ukweli usiopingika.

Ikumbukwe kuwa muziki wa kizazi kipya ndio unaanza muongo wa pili tangu uanze kukubalika na jamii na sasa angalao wanaokuja wanaanza kula matunda ya kazi za sanaa hasa muziki huu wa kizazi kipya. Kwangu mimi kama mpenda burudani siko upande wowote kati ya hizi mbili lakini najaribu kujiuliza kama Lady Jay Dee ni mwanamuziki mkubwa na anajiweza angalao kifedha akiwa na vijimiradi kadhaa anataabika namna hii iweje wale wasio na uwezo na soko bado halijawakubali masharti wanayokutana nayo.

Sio mara ya kwanza kwa walalamikiwa kulalamikiwa hivi na wasanii waliothubutu, ni wazi kuwa wapo mashabiki wengi na wanahabari ambao pia wanaogopa kuandika chochote kuhusiana na yanayolalamikiwa ama kwa maslahi binafsi au kwa hofu ya kuwa walalamikiwa ndio “baba” wa Burudani Bongo!!

Wakati imetokea Mheshimiwa Mbunge wa Mbeya Mjini Mr Sugu kusuguana na Ruge mpaka kupelekea kuwa na pande mbili za wanaburudani niliwahi kuliandikia suala lile na kumuomba waziri anayehusika ajaribu kulivalia njuga na kuwakalisha chini wahusika kujaribu kutoa tofauti zao (isome hapa), wakati huo Waziri alikuwa Mh. Emanuel Nchimbi na hatimaye aliwaita na kukaa nao chini ikiwa baada ya Mixtape ya Anti Virus kutoka ikiwa na wanamuziki kibao ambao walishambulia vilivyo walalamikiwa wa Jay Dee hii leo.

Hakuna anayebisha kuwa ukitaka kitu chako kifanikiwe basi washirikishe Clouds na hapo utafanikiwa sana, lakini ikumbukwe kuwa kwenye wengi kuna mengi wapo wengine ambao watakuwa na mlengo wa kushoto ambao hawawezi kukubaliana na mifumo iliyopo kama ilivyo kwenye Siasa, wapo watakao ridhika na wapo ambao hawataridhika, kwa nafasi iliyonayo Clouds kwa sasa na kwenye sura ya jamii ingejitahidi kuweza ku accommodate makundi yote mawili, wanachogombea Jay Dee na Clouds ni mgogoro wa Kimaslahi tu ambao wote wakikaa chini unaweza kutatuliwa.

Madhara ya migogoro hasa ikihusisha watu majemedari kwenye burudani kama Ruge, Jose na Jay Dee ni wazi inagawa hata wanamuziki wenyewe, mashabiki na hatimaye vyombo vya habari. kwani moja ya malalamiko ya JAy Dee ni kuwa wanamuziki wamepigwa mkwara kutoa nyimbo zikimhusisha Lady Jay Dee kwani hazitapigwa na hawatajumuishwa kwenye matamasha yaliyoandaliwa na walalamikiwa, kwangu mimi hili ni pigo si tu kwa Jay Dee bali hata kwa mashabiki ambao kwa sasa kutokana na mitandao ya kijamii wanamuziki wamekuwa karibu sana na mashabiki wao mathalani mashabiki wanaweza kutaka kumuona Jay Dee akipiga na Diamond itakuwaje? na kumpa changamoto ambayo akiifanyia kazi na kuwaridhisha mashabiki wake, Kwangu mimi ugomvi huu unawaathiri mpaka mashabiki wa Muziki wa JAy Dee, na hata biashara za Jay Dee pia, mathalani kwa shabiki ambaye anajua kuwa anajulikana na pande zote mbili leo hii hawezi kwenda Nyumbani Lounge akihosfia kuona na habari kufika si kwa shabiki tu bali hata wanamuziki wenyewe.

Hali hii haina afya hata kidogo kwa uhai wa muziki wetu, Kwani kwa sasa Muziki unaajiri vijana wengi zaidi jambo linalopelekea kupunguza tatizo kubwa la ajira kwa vijana.

Sasa kwanini tufikie hapo? ni bora kuwakalisha hawa wawili na naamini kabisa Waziri husika anaouwezo wa kufanya hili kwani Waziri mwenyewe ni kijana na jambo hili linagusa wadau wake kwa kiasi kikubwa. kwani wengi wa waathirika kwa namna yeyote ile ama iwe upande wa Jay Dee au upande wa Taasisi ambazo zinamhusu Ruge kibinafsi au kikazi waathirika bado ni vijana. Mheshimiwa Waziri wa Vijana na Michezo Fenela Mkangara na Naibu wako Amos Makala jukumu liko kwenu kutuondolea aibu hii kwenye sekta ya burudani.

Nakuacha na kibao Mtu pesa cha Twanga Pepeta, pata burudani.


%d bloggers like this: