Buriani Baba Kruvet.

June 18, 2012

Willy Edward 1974 – 2012

Nilipokea taarifa za msiba wa Willy Edward kwa masikitiko makubwa toka kwa Michuzi akiwa ameandika kwenye status yake ya facebook. Nilishtuka kwa vile Willy ni mtu si tu ninayefahamiana naye bali niliwahi kufanya naye kazi ofisi moja pale Business Times – Majira. Enzi hizo mi nikiwa head wa Production Department ya Matangazo ya Business Times, Majira, Maisha, Dar Leo, Sanifu na Spoti Starehe.

Willy Edward alifariki dunia Ghafla usiku wa kuamkia Jumamosi huko Morogoro, Hadi sasa hatujapata taarifa rasmi za kidaktari kuhusu kifo chake, lakini taarifa zilizopatikana kutoka kwa ndugu wa marehemu zinasema alikuwa anasumbuliwa na tatizo la moyo.

Wakati huo nikiwa nikiwa Business Times, Willy tulikuwa wote tunasimamamia production ya Gazeti kuhakikisha kila kitu kiko sawa nakisha tunapeleka kurasa za gazeti wote kiwandani kwenye Printing wakati ofisi zikiwa Mtaa wa Bibi Titi na Kiwanda kikiwa Lugoda, yeye ndiye alikuwa akipeleka na kusimamia kurasa za editorial na mimi nikisimamia kurasa za matangazo, ni mtu ammbaye nilikuwa nafanya naye kazi kwa karibu kwani sisi pekee ndio tulikuwa watu wa mwisho baada ya maandalizi yote lazima tupeleke Pages kiwandani ndipo tunarejeshwa makwetu, na bila page zake basi za kwangu haziendi pia bila zangu za kwake haziendi na gazeti halitoki pia. Mzunguko huu ulinifanya kuwa karibu naye sana kwani baada ya hapo tunapanda gari na yeye anaanza kushuka kisha sie wengine humo njiani mnacheka na kupiga soga sana.

Willy alikuwa mshabiki sana wa michezo hasa mpira wa miguu, kiasi mtoto wake alimuita Kruvert jina la mchezaji wa Uholanzi Patric Kruvert na mi kila mara nilikuwa nikimuona namuita Baba Kruvert na ye kuniita Papaa kwa sababu napenda sana Lingala na muziki wake.

Willy Alifanikiwa kuaminika na kutokana na uwezo wake kazini alipanda daraja na kuwa Mhariri wa gazeti la Dar Leo kuanzia mwaka 2002 hadi 2005.

Kipindi cha mwaka 2006 hadi 2007 alikuwa akitumikia nafasi ya Mhariri wa Msaidizi wa Michezo gazeti la Majira na baadaye 2006 hadi 2007 akawa Mhariri wa Michezo wa gazeti hilo. Kisha alipanda na kuhamia vyombo mbalimbali kabla ya 2010 kujiunga na Jambo Leo.

Baada ya pilikapilika za Busniness Times mi nilitoka kwenye magazeti lakini nikiwa bado na mahusiano ya karibu sana na Willy huku akiniandikia makala mbali mbali za huku ninakofanyia kazi na pia Willy alikuwa mshabiki mkubwa wa Bolingo hasa JB Mpiana na alikuwa shabiki mkubwa wa blogu hii ya Spoti na Starehe na hivi karibuni tulikuwa na mpango wa kunipa Half Page ambayo ningekuwa naandika kuhusu muziki wa Congo kwenye gazeti la Jambo Leo ambalo marehemu alikuwa akifanyia kazi, tumekuwa tukiliongea hili mara kwa mara mpaka layout ya page tumeishaijadili na tulichokuwa tunajadili cha mwisho kabla ya kuanza ni heading ya page yangu.

Hili kwangu ni pigo kwani napenda sana kuandika na yeye tulikuwa tunaelewana sana na kuna wakati tulikuwa tukiandika makala hizi za Muziki wa Kongo pamoja na yeye na Frank Sanga.

Mara ya mwisho nilikutana na Willy tukiwa Airport mi nikielekea Malaysia na yeye akielekea Uturuki, tuliongea sana mpaka tulipoaachana na kuendelea kuwasiliana pia. Willy ameondoka huku akianza kufikia ndoto ambayo waandishi wengi wanaitaka, akiwa Mhariri wa Gazeti ambalo lilikuwa linakuja juu kwa kasi na kujiimarisha sokoni na kwa wasomaji, Gazeti la Jambo Leo ambalo linaongozwa na timu ya waandishi wachapakazi vijana.

Ni dhahiri jumuiya ya waandishi wa Habari imempoteza kijana mchapakazi ambaye uweledi wake katika fani ungekuwa darasa tosha kwa yoso wanaokuja na kuchipukia kwenye tasnia hii ya Habari.

Habari zinasema Willy atasafirishwa kwenda kuzikwa kwao huko Musoma

mkutano wa Jukwaa la Vyombo vya
Habari Afrika na Uturuki


%d bloggers like this: