Adebayor ajiunga Real lMadrid kwa mkopo

January 27, 2011

Mshambuliaji wa Manchester City Emmanuel Adebayor amejiunga kwa mkopo na klabu ya Real Madrid hadi mwishoni mwa msimu huu. Emmanuel Adebayor Mshambuliaji wa zamani wa timu ya taifa yaTogo, anatazamiwa kuelekea Hispania siku ya Jumatano kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa afya yake katika klabu hiyo. Madrid watakuwa na uchaguzi kama watahitaji kumnunua moja kwa moja Adebayor mwenye umri wa miaka 26 mwishoni mwa msimu, wakati mkataba wake wa mkopo utakapomalizika. Adebayor alijiunga na Manchester City akitokea Arsenal kwa kitita cha paundi milioni 25 mwaka 2009 na ameshafunga mabao 19 katika michezo 36 ya ligi na mashindano mengine katika Manchester City. Anakuwa mshambuliaji wa pili mwandamizi wa Manchester City kuondoka katika klabu hiyo katika kipindi cha miezi sita, baada ya Robinho kwenda AC Milan na anaonekana atamsaidia meneja wa Real, Jose Mourinho kuziba pengo la mshambuliaji Gonzalo Higuain, anayesumbuliwa na matatizo ya mgongo. Kabla ya kumtupia jicho Adebayor, Real ilijaribu kumsajili mshambuliaji wa Hamburg, Ruud van Nistelrooy, huku dau lao la paundi milioni 39 likikataliwa kwa kutaka kumchukua mpachika mabao wa Atletico Madrid, anayechezea pia timu ya taifa ya Argentina, Sergio Aguero. Adebayor ataweza kucheza mashindano ya Ligi ya Ubingwa wa Ulaya na pia ligi ya Hispania, maarufu La Liga, Reala Madrid wakiwa wanashikilia nafasi ya pili, na iwapo mambo yake yatakwenda vizuri huko Bernabeu, anaweza kusaini mkataba wa kudumu kwa dau la uvumi la paundi karibu milioni 15.

Advertisements

%d bloggers like this: